Jamii ya Nyatieko Yaungana Kumsaidia Kijana Aliyenyang'anywa Shamba na Familia

Jamii ya Nyatieko Yaungana Kumsaidia Kijana Aliyenyang'anywa Shamba na Familia

Na Mwana wa Afrika 

Wakaazi kijiji cha Mwanyarang'o, kitongoji cha Mwamisioma, kaunti ya Kisii, wameungana kumsaidia kijana James Onchwari Maisiba, ambaye alifukuzwa kutoka kwenye shamba la familia yake baada ya wajomba zake kuuza ardhi hiyo. 

Hatua hii ilichukuliwa  baada ya kijana huyo kukumbwa na masaibu ya kufukuzwa mara tu baada ya kifo cha babake.

James, akieleza hali yake, alisema kuwa aliambiwa aondoke kwenye shamba hilo na wajomba zake waliouza ardhi hiyo bila idhini yake. 

"Mimi nilikuwa hapa tangu baba yangu alipokuwa akipumzishwa, lakini kwa sababu ya maneno mawili matatu, wajomba zangu waliungana na kuuza shamba hili na kuniambia niondoke," alisema kwa masikitiko.

James Onchwari Maisiba

Licha ya changamoto hizi, wakaazi wa kijiji hicho, pamoja na machifu wa eneo hilo, waliamua kuchukua hatua ya kumjengea nyumba kijana huyo kwenye shamba hilo. Hatua hiyo ilifanyika hata baada ya ardhi hiyo kuuzwa, ikiwa ni ishara ya mshikamano na umoja katika jamii hiyo.

Mmoja wa wakaazi wa kijiji hicho alizungumza na vyombo vya habari, akibainisha kwamba kijana James alizaliwa na kukulia katika shamba hilo, na hivyo hawangeweza kuruhusu aondoke bila msaada. 

"Sio mara ya kwanza kupigania haki za kijana huyu. Mara ya kwanza walifunga nyumba yake, na baadaye tukarudi na maafisa pamoja na chifu na kufungua. Hii ni mara ya pili tumeamua kupigania haki yake. Ni mmoja wetu katika kijiji hiki na hatuwezi ruhusu tena wajomba wake kumfukuza," alisema mmoja wa viongozi wa kijiji hicho.

James, akionyesha shukrani zake kwa jamii, alisema, "Nashukuru sana wanajamii pamoja na chifu kwa sababu ya kazi nzuri waliyofanya kwa ajili yangu."

Chifu wa eneo hilo alithibitisha kwamba kijana James ataishi rasmi katika shamba hilo, ambalo ni sehemu yake ya kuzaliwa na kulelewa.