Kisii: Ubomoaji wa Vibanda Daraja Moja Waacha Wafanyabiashara na Hasara

Kisii: Ubomoaji wa Vibanda Daraja Moja Waacha Wafanyabiashara na Hasara

Mwana wa Africa 

Wafanyabiashara katika mji wa Kisii, sehemu za Daraja Moja kwenye barabara ya Jogoo, wamekadiria hasara leo baada ya shirika la ujenzi wa barabara (KenHa) kubomoa vibanda vilivyokuwa katika maeneo hayo, ambavyo inasemekana vilijengwa kwenye maeneo ya upanuzi wa barabara.

"Kwa sasa hakuna kazi tena Daraja Moja. Tutaenda wapi? Gavana anasema kazi ipo, lakini hakuna kazi hapa nje... tutaenda wapi kesho? Tutatoa wapi unga? Tukienda maandamano, mnasema tunaharibu mali... Kazi iko wapi? Tutafanya nini?" Boni alieleza.

Vijana ambao wamekuwa wakitegemea sehemu hiyo kwa miaka mingi sasa wamelalamikia serikali, wakisema kuwa sehemu hiyo ndiyo iliyokuwa ya kipekee na imekuwa ikiwasaidia kupata pesa za kujikimu kimaisha na hata kusaidia familia zao.

"Nimekuwa nikifanya kazi hapa kwenye sehemu ya uoshaji wa magari. Leo nimeamka kama kawaida kufungua kazi, na vile mnavyoona hali imekuwa tofauti. Sasa swali ni moja... vijana kama sisi tumekuwa tukitegemea kazi hii, angalau kupata shilingi ili kununua sabuni, nguo, lakini kwa sasa hakuna tena... nauliza serikali tutaenda wapi? Na tukiandamana, mambo ni yale yale," alisema Bonni, mmoja wa wafanyabiashara.

Aidha, shirika la KenHa limetekeleza haya ili kuandaa upanuzi wa barabara katika sehemu hiyo mjini Kisii. Inasemekana kuwa wafanyabiashara hao walikuwa wamepewa onyo miaka miwili iliyopita kuhusu ubomoaji wa vibanda hivyo.