Makwata Aiadhibu Shabana; Kenya Police Yaboronga

Makwata Aiadhibu Shabana; Kenya Police Yaboronga

Na Mwana wa Africa

 

Timu ya Kariobangi Sharks ilitoka nyuma na kuwaziba Shabana FC 2-1 katika uwanja wa Dandora siku ya Jumamosi Mei, tarehe 18 saa tisa alasiri. 

Johnmark Makwata katika ubora wake, aliiendelea kuzima matumaini ya shabana kusalia katika ligi kuu ya KPL msimu ujao baada ya kufunga mabao mawili chini ya dakika tatu.

Licha ya Shabana kutilia mkazo kwenye mchezo, Makwata alisawazisha dakika ya 78 na kuongeza la pili katika dakika ya 79. Kwa sasa mchezaji huyo ambaye anawinda taji la  mfungaji bora wa msimu, ana magoli 13 chini ya mechi 9 ambazo amecheza. Anawafuata kwa ukaribu Benson Omalla (Gor Mahia) na

 Tito Okello (Police FC) ambao wana mabao 15 kila mmoja. 

Ushindi huo wa 2-1 umewafanya kupanda kwenye jedwali kutoka  nafasi ya tisa hadi ya saba kwa alama 44, alama mbili nyuma ya Nairobi City Stars ambao watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Nzoia Sugar ambayo huenda ikashuka daraja msimu huu. 

Kutokana na matokeo hayo, vijana wake kocha Pamzo wameshikilia nafasi ya 17 kwa alama 29, alama mbili  nyuma ya Sofapaka ambayo itachuana wiki hii na  Bandari FC siku ya jimipili  katika uwanja wa Ukunda Showground. Wapo mbele ya Muhoroni Youth kwa alama moja pekee.

Katika matokeo mengine ni kuwa Police imeshuka kwenye jedwali baada ya kupoteza mechi zake mbili mfululizo dhidi ya AFC Leopards na Tusker FC.  Police walipoteza 1-0 dhidi ya Leopards katikati mwa juma na Jumamosi 18,  wakapoteza 1-0 dhidi ya Tusker FC.

Bao la Charles Momanyi, liliwasaidia Tusker kusimama nafasi ya pili kwenye jedwali kwa alama 55, alama moja mbele ya Police FC na nane nyuma ya vinara Gor Mahia ambao jumapili wataumiza nyasi katika uwanja wa Sportpesa Arena  na Muhoroni  Youth saa tisa alasiri.  

Kakamega Homeboyz ilishuka kwenye jedwali hadi nafasi ya nane  baada ya kupoteza 2-1 dhidi ya Posta Rangers katika uwanja wa Police Sacco Stadium.