Miaka 60 ya Uhuru: Wakenya Wasisitiza Changamoto za Kiuchumi, Vijana Wapoteza Matumaini
Japo wakenya wamesherehekea miaka 60 ya kujitawala, hawana matumaini kabisa kwa kulemewa na gharama ya maisha.
By Seliphar Machoni
Inapendeza kuona jinsi Kenya imepiga hatua katika miaka 60 ya uhuru wake.
Hata hivyo, inaonekana kuna tofauti kubwa kati ya mtazamo wa rais Wiliam Ruto na wananchi wa kawaida.
Rais Ruto anadai uchumi umestawi, lakini wengi wa wananchi, hasa vijana, wanalalamikia kupanda kwa gharama ya maisha.
Wakati wa sherehe za uhuru, zilizoandaliwa mjini Nairobi, rais alipongeza mafanikio ya sera zake za kiuchumi.
Vijana kote nchini ambao ndio asilimia 75 ya raia wa Kenya, uhuru kwao ungali ndoto huku hata waliosoma hadi vyuo vikuu wakishindwa kupata riziki.
Wakitoa maoni yao baadhi ya vijana kutoka katika kaunti ya Kakamega, wanalaumu kupanda kwa bei ya bidhaa kama vile unga na sukari, wakisisitiza kuwa hawajapata kunufaika na ukuaji wa uchumi unaodaiwa.
Pia, wanaonyesha wasiwasi wao kuhusu ongezeko la ushuru, wakisisitiza kuwa linafanya maisha yawe magumu zaidi. Wanasema hawajayaona matunda ya ahadi za rais kuhusu ajira na fursa za maendeleo kwa vijana.
Japo Wakenya wamesherehekea miaka 60 ya kujitawala, hawana matumaini kabisa kwa kulemewa na gharama ya maisha, ukosefu wa ajira, kukabiliana na njaa, maradhi, na kushindwa kulipia karo watoto wao kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.
Wataalamu wanasema kwamba Kenya haina uwezo wa kulisha raia wake kwa namna toshelevu miaka 60 baada ya kujikokboa kutoka ukoloni.
Tukirudi katika uongozi wa hapo awali na maraisi waliotangulia, wengi walikuwa na sera na mipangilio kabambe ya kudhibiti njaa nchini.
Bw. Timothy Njagi, mtafiti katika Tegemeo Institute of Agriculture Policy and Development, anasema kwamba kuna watu wengi wanaolala njaa nchini Kenya hata katika maeneo ya mijini. Idadi hii imeongezeka miaka iliyopita kwa sababu ya janga la Korona, ukame, na hali ya sasa ya mfumko wa bei ya vyakula, huku mapato yakipungua kwa wale wanaofanya vibarua.
“Tatizo pia linatokana na ukweli kwamba watu wengi katika maeneo ya miji hawapandi chakula, na kwa hivyo, wanapokosa mapato ya kununua, hulazimika kupunguza mlo,” asema Njagi.
Hata hivyo, wanaosoma hadi vyuo vikuu hawapati ajira, na wanaofanya vibarua wanalemewa na gharama ya juu ya maisha inayoshuhudiwa nchini kwa wakati huu.
Sera za serikali ya sasa ya Kenya Kwanza zinaonekana kuenda kinyume na ndoto ya waanzilishi wa taifa la Kenya za kuwezesha raia kuwa na maisha bora kuliko waliyokuwa nayo chini ya utawala wa kikoloni. Na pia kuenda kinyume na matarajio ya wakenya ambao walikuwa na matumaini makubwa kwa serikali hii.
Serikali imekumbatia mikopo kutoka mashirika yanayodhibitiwa na nchi za Ulaya yanayotoa masharti makali yanayoumiza raia wa kawaida kwa kumbebesha mzigo mkubwa wa ushuru.
“Kwa mujibu wa takwimu, Kenya inakabiliwa na tatizo la ongezeko la vijana, huku makadirio yakionyesha kuwa asilimia 75 ya wakazi wa Kenya wana umri wa chini ya miaka 35.
Ukosefu wa ajira kwa vijana nchini unasemekana kuwa juu hadi asilimia 35 (takriban vijana na wanawake milioni 4.5 hawana ajira), ikilinganishwa na kiwango cha ukosefu wa ajira kitaifa cha asilimia 10.
Katika mwaka mmoja uliopita, Wakenya kadhaa wamepoteza kazi.
Shirikisho la Waajiri nchini (FKE) lilishutumu kuongezeka kwa gharama ya uzalishaji nchini, huku likionya kuwa maelfu ya Wakenya watakosa kazi iwapo sera za serikali kuhusu ushuru hazitabadilishwa.