Mwanzo Mgumu kwa Malkia Strikers Kupoteza Dhidi ya Brazil Katika Paris 2024
Na Mwana wa Afrika
Timu ya voliboli ya Malkia Strikers ilianza mashindano ya Paris 2024 nchini Ufaransa kwa kichapo cha seti tatu kwa bila siku ya Jumanne saa nane mchana kutoka kwa timu ya Brazil katika uwanja wa South Paris Arena.
Washindi mara mbili wa Brazil walionekana kuwazidi nguvu Malkia Strikers katika seti ya kwanza ambapo waliwapepeta 25-14.
Licha ya Malkia Strikers kuwa na tumaini katika seti ya pili, vipusa wa Brazil walirejea kwa vishindo na kuwashinda 25-13 na hatimaye kumaliza seti ya tatu kwa ushindi wa 25-12.
Licha ya safu ya ushambulizi ya Malkia Strikers kujitahidi, vipusa hao wa Brazil waliweza kuwazuia ipasavyo kutokana na uzoefu wao.
Kwa sasa, vipusa wa Brazil wameweka historia ya kutopigwa na Kenya mara nane katika mechi ambazo wamekutana, ikiwemo kwenye Kombe la Dunia na Olimpiki. Kwa jumla, Malkia Strikers wamepoteza mara ishirini na moja dhidi ya Brazil.
Aidha, vipusa wa Kenya wanatarajiwa kufanya vyema katika kundi B kwenye mechi yao ya pili siku ya Jumatano, 31 dhidi ya Poland, ambao walianza mashindano kwa ushindi wa 3-1 dhidi ya Japan katika mechi yao ya ufunguzi.