Panda Shuka za Bidhaa Sokoni
Baadhi ya bidhaa za vyakula zimepanda maradufu katika soko la Daraja Mbili, Kaunti ya Kisii, kutokana na uchumi nchini ambao umekuwa katika hali ya panda shuka.
Bidhaa hizo ni pamoja na nafaka na matunda. Baadhi ya bidhaa hizi ni kama vile ndengu, maharage, pojo, ndimu, machungwa, na maharagwe.
Ndimu, gunia moja, zinauzwa kwa shilingi 2,000 kutoka 1,500. Ndimu hizi husafirishwa kutoka Busia, Pokot, na nchi ya Uganda pamoja na sehemu zingine. Sokoni humo, ndimu nne huuzwa kwa shilingi 30, na ndimu moja huuzwa kwa shilingi 10, hali hii hutegemea na wauzaji ambao hupata faida ya shilingi 200 hadi 500 kwa kila gunia.
Machungwa aina ya Seedless, gunia moja lenye kilo sabini, kuuzwa kwa shilingi 7,600 kutoka 7,000, huku kreti moja yenye machungwa ikiuzwa kwa shilingi 2,400 kutoka 2,000. Machungwa haya, ambayo yanaaminika kutokuwa na mbegu, yanauzwa matano kwa shilingi 100, huku chungwa moja likiuzwa kwa shilingi 20. Sawia na ndimu, biashara hii huuzwa kutegemea na ukubwa wa chungwa.
Wimbi au pojo, kilo tisini kwa gunia, huuzwa kwa shilingi 16,000 kutoka 15,600-15,800 ambapo muuzaji huuza gorogoro moja kwa shilingi 300. Tofauti na mchele, kilo sitini huuzwa kwa shilingi 6,000 huku gorogoro moja ikiuzwa kwa shilingi 300.
Mwanabiashara wa pojo hupata faida ya shilingi 1,500-2,000 na zaidi kwa kila gunia, naye wa mchele hupata faida ya shilingi 800-1,000 na zaidi kwa kila gunia.
Mohogo, kilo 120, huuzwa kwa shilingi 4,000 kutoka 3,500, huku gorogoro moja ikiuzwa kwa shilingi 60. Nayo maembe mabichi, gunia dogo, yakiuzwa kwa shilingi 850 kutoka 700, tofauti na maembe yaliyoiva ambayo huuzwa kwa shilingi 1,800 kutoka 1,600 kwa kila kreti moja.
Kilo tisini ya gunia la maharage aina ya Onyoro yanauzwa kwa shilingi 7,500 kutoka 7,000, huku gorogoro moja ikiuzwa kwa shilingi 250 kutegemea na mnunuzi. Tofauti na kilo tisini ya maharage aina ya Amini ambayo huuzwa kwa shilingi 9,800 kutoka 9,000, na gorogoro moja ya maharage haya huuzwa kwa shilingi 300.
Kilo tisini ya maharage aina ya Green-Yellow huuzwa kwa shilingi 14,000, huku gorogoro moja ya maharage haya ikiuzwa kwa shilingi 450/430.
Gorogoro moja ya maharage aina ya Amini-Grade na Yellow-Mayai yanauzwa kwa shilingi 350 kila aina, japo kilo tisini ya maharage ya Amini-Grade inauzwa kwa shilingi 12,800 kutoka 12,500, nayo aina ya Yellow-Mayai inauzwa kwa shilingi 9,000 kutoka 8,500.
Kilo tisini ya maharage aina ya Matumbo yanauzwa kwa shilingi 12,000, huku gorogoro moja ya maharage hayo ikiuzwa kwa shilingi 450, sawia na maharage aina ya Rosecoco, ambapo kilo tisini huuzwa kwa shilingi 13,500 kutoka 13,000, na mkebe mmoja kuuzwa kwa shilingi 450.
Biashara hii ya uuzaji na ununuzi wa nafaka, matunda, mboga, na bidhaa nyinginezo katika soko la Daraja Mbili hutegemea mbinu ambazo wauzaji hutumia katika biashara zao.