Shule za Musingu na Kakamega zazika tofauti zao

Shule za Musingu na Kakamega zazika tofauti zao
Wachezaji wa timu ya Musingu na ile ya Kakamega

Na Getiro Vincent

 

Hatimaye vuta nikuvute kati ya shule ya upili ya wavulana ya Kakamega na ile ya Musingu kuhusu uhamisho wa wanafunzi wa

soka baina ya shule hizo mbili uliofanyika mwezi wa kumi mwaka uliopita umefikia tamati baada ya walimu wakuu wa shule hizo mbili kukutana na kupata suluhu.

Mkurugenzi wa elimu katika kaunti ya Kakamega Hellen Nya'angau aliyeongoza kikao hicho cha kutafuta suluhu, alidhibitisha haya na kusema kuwa uchunguzi uliofanywa haukupata dosari yoyote katika uhamisho wa wanafunzi saba kutoka shule ya Kakamega hadi ya Musingu.

"Ni ukweli wanafunzi tisa wa soka kutoka shule ya wavulana ya Kakamega walifanyiwa uhamisho mwaka jana kwenda kusomea Musingu. Baada ya kufanya uchunguzi, tulipata wawili kati ya hao tisa hawapo katika shule hiyo tena. Mmoja alirejea katika shule ya Kakamega na mwingine alienda kwao Nyanza kupata matibabu kutokana na ugonjwa. Wanafunzi saba waliobaki katika shule ya Musingu wanasoma katika vidato tofauti na wamelipiwa karo yao ya mwaka mzima ila hawajakamilisha uhamisho huo kikamilifu," alidhibitisha Nya'angau.

 

Nya'angau amepongeza walimu wakuu hao kwa kukubaliana na kuwataka washirikiane kuhakikisha wanafunzi waliohamishwa wanaendeleza masomo yao bila tatizo.    

 

"Kulingana na sheria ya KSSA, ni wanafunzi wawili pekee waliohamishwa kutoka shule moja ndio wanaruhusiwa kuichezea timu ya Musingu na wakizidi wawili itakuwa ni kinyume na sheria. Wanafunzi tano wanaosalia wataichezea timu ya Musingu baada ya kukamilisha mwaka mmoja katika shule hiyo. Hamna tatizo lolote kwa wanafunzi kuhamishwa kutoka shule moja hadi nyingine ili mradi sheria imefwatwa kwenye mchakato huo," alisema Nya'angau.

Aidha, walimu wakuu wa shule zote mbili walionekana kuridhishwa na uamuzi huo na kusema kuwa wanajiandaa kwa mashindano ya michezo ya sekondari ngazi ya kaunti ambayo yameratibiwa kuanza tarehe nne hadi sita mwezi wa saba.

Julius Mambili, Mwalimu mkuu wa shule ya wavulana ya Kakamega, ambayo iliwasilisha malalamishi ya uhamisho huo,

alisisitiza kuwa, "uamuzi huo ni halali na kama shule hatuna lolote la kufuatilia tena. Kwa sasa tunatayarisha timu yetu ya soka kabla ya mashindano hayo,"

Kwa upande wake Benard Lukuya, ambaye ni mwalimu mkuu wa shule ya Wavulana ya Musingu, alimuunga mkono mwalimu mkuu mwenza.

 

"Uchunguzi umedhibtisha kuwa sheria ilifwatwa. Kwa sasa tumezika tofauti zetu na tayari timu zote mbili zimewasilisha stakabadhi za wanafunzi watakaoshiriki michezo mwezi ujao. Sote tumekubaliana kuenda kuboresha vikosi vyetu,"

 

Wawili hawa wamewataka mashabiki wao kuzingatia utulivu na amani kabla na wakati wa mashindano hayo ikizingatiwa kuwa timu hizo mbili, ambazo zimejumuishwa katika kundi la A, zitakutana katika mchezo wao kwanza.

 

"Hakuna uhasama wowote baina yetu na ndio sababu tunafurahia kufika kiwango hiki. Shule hizi mbili zina historia ya kuletea kaunti ya Kakamega sifa nzuri. Tunaomba wapenzi wetu wa soka wawe na amani wanapojiandaa kwa michezo ya kaunti. Sote tutaunga mkono timu itakayoshinda kwenda kutuwakilisha katika kiwango cha mkoa wa magharibi," walisema Mambili na Lukuya.