Ukarabati wa Uwanja wa Gusii Kufika Tamati
Na Mwana wa Afrika
Ukarabati wa Uwanja wa Gusii ulioko katika mji wa Kisii unaelekea kukamilika baada ya ujenzi wa muda mrefu wa uwanja huo.
Timu ya Shabana FC, ambayo ilitumia uwanja huo kama uwanja wa nyumbani katika ligi ya daraja la chini, huenda ikautumia tena uwanja huo kwa mechi yake ya ufunguzi dhidi ya Kenya Police au Posta Rangers ligini.
Uwanja huo, wenye uwezo wa kubeba zaidi ya watu elfu tano, umefanyiwa marekebisho makubwa na sasa unafuata sheria na kanuni za FKF, tofauti na hali ilivyokuwa awali.
Vijana wa kocha Pamzo walilazimika kutumia Uwanja wa Raila Odinga ulioko katika Kaunti ya Homabay kama uwanja wa nyumbani msimu uliopita, baada ya Uwanja wa Gusii kukosa kufikia viwango vinavyohitajika ili kuruhusiwa kutumika katika Ligi Kuu nchini. Mashabiki wa Tore Bobe walisema hali hiyo ilichangia matokeo duni kwa timu yao msimu uliopita.
Licha ya ukarabati ulioendelea, Uwanja wa Gusii ulitumika katika mwezi wa saba na wa nane kuandaa mechi za sekondari za KSSSA Nyanza katika michezo ya kanda na ile ya kitaifa.
Tore Bobe wana matumaini ya kusajili matokeo bora iwapo watautumia Uwanja wa Gusii kama uwanja wa nyumbani msimu huu, sawa na walivyofanya katika ligi ya daraja la chini, NSL.