Waandishi wa Habari Kaunti ya Kisii na Nyamira Wapinga Ukatili wa Polisi

Waandishi wa Habari Kaunti ya Kisii na Nyamira Wapinga Ukatili wa Polisi

Na Mwana wa Afrika

Kufuatia wito wa kitaifa kwa waandishi wa habari kupinga ukatili wa polisi dhidi ya vyombo vya habari, jamii ya waandishi wa habari kutoka kaunti ya Kisii leo imefanya maandamano ya amani katika mji wa Kisii kuonyesha kutoridhika kwao na ukatili wa polisi dhidi ya wanahabari, hasa katika maandamano ya Gen Z.

Waandishi wa habari walikuwa wakiimba nyimbo za uhuru wa vyombo vya habari walipokuwa wakielekea ofisi ya kamanda wa polisi wa kaunti ya Kisii, Charles Kasses.

Vyombo vya usalama katika kaunti ya Kisii vimewahakikishia waandishi wa habari usalama wao wakiwa kazini na kuwajulisha kuwa haki zao zimewekwa katika katiba ya Jamhuri ya Kenya. Kaimu Naibu Kamishna wa Kaunti ya Kisii Central, Felistus Ndinda, amewahakikishia wanahabari kuwa haki zao zitafuatwa pamoja na uhuru wao katika kaunti hiyo.

"Tutahakikisha waandishi wa habari wote wamelindwa na haki zao zimefuatwa ipasavyo," alisema Ndinda.

Aidha, waandishi wa habari wa Nyamira pia walijiunga na nchi nzima kuandamana dhidi ya polisi kutumia nguvu na risasi dhidi ya waandishi wa habari wakati wa maandamano ya Gen Z. Waandishi hao wa habari waliandamana kutoka steji ya Nyamira hadi ofisi ya kamanda wa polisi wa kaunti, ambapo walihutubiwa na kamanda wa polisi wa kaunti, Agnes Amojong, kuhusu usalama wa waandishi wa habari katika kaunti ya Nyamira.

"Kufuatia kesi ambazo zimekuwa zikiripotiwa kuhusu wanahabari, tutahakikisha sheria za wanahabari zimefuatwa na wamelindwa kwa ajili ya usalama wao," alisema Amojong.

Sasa wanatoa wito kwa waandishi wa habari kupewa uhuru wao na kulindwa dhidi ya kulengwa na polisi wakati wa maandamano ya kupinga serikali.