Wanafunzi wa Chuo Kikuu Kisii Wakosa Kuhitimu Kwa Kukosa Alama

Wanafunzi wa Chuo Kikuu Kisii Wakosa Kuhitimu Kwa Kukosa Alama
Wanafunzi wapanga foleni ili kupata huduma

Katika mchakato wa kuhitimu, furaha ya takriban asilimia ishirini ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kisii hugeuka kuwa karaha wanapokumbana na tatizo la alama zao kukosekana. 

Changamoto hii inasitisha vijana wenye ndoto za kufanikiwa, wakilazimika kuzunguka afisi za chuo bila majibu. Je, nini hasa kinachozuia ndoto zao kutimia?

Katika vyuo vikuu vingi nchini Kenya, changamoto mbalimbali huwazuia wanafunzi wanapokaribia kukamioisha masomo yao. 

Katika Chuo Kikuu cha Kisii, mojawapo ya matatizo yanayowakumba wanafunzi wanaotarajia kuhitimu ni alama zao kukosekana kwenye rekodi za mitihani. 

Tatizo hili limekuwa kero kubwa kwa wanafunzi wengi, mara nyingi likisababisha kucheleweshwa kwa mahafali yao au hata kupoteza mwaka wa masomo. Ni kikwazo kikubwa kinachokatisha tamaa na ndoto za vijana wengi.

Tatizo hili linahusishwa na mifumo duni ya usimamizi wa deta chuoni. Inadaiwa kuwa alama hupotea kutokana na hitilafu katika uwasilishaji wa matokeo kutoka kwa wahadhiri kwenda kwa ofisi ya mitihani. Baadhi ya wanafunzi wanalalamika kuwa wahadhiri wao hawakuwasilisha alama kwa wakati au walipoteza karatasi za mitihani, hali inayowafanya wanafunzi kubaki njia panda.

Mwanafunzi mmoja, aliyeomba jina lake lisitajwe kwa kuhofia kunyanyaswa, alieleza machungu yake. 

"Nimekuwa nikikimbizana na idara kwa miezi kadhaa. Kila mara nikiuliza kuhusu alama zangu, naambiwa nirejee baadaye. Inaumiza kwa sababu nimejitahidi sana, lakini sasa naona ndoto zangu zinacheleweshwa," alisema kwa huzuni.

Madhara ya Kukosekana kwa Alama

Kukosekana kwa alama si tu kunawachelewesha wanafunzi, bali pia kunawafanya wapoteze muda mwingi wakifuatilia suala hilo badala ya kuendelea na mipango yao ya baada ya chuo. Wanafunzi wengi wanalazimika kutembelea idara zao mara kwa mara bila kupata suluhisho. Hali hii inawafanya wajihisi kama hawathaminiwi na uongozi wa chuo.

Baadhi ya wanafunzi pia hukosa fursa muhimu za mafunzo ya kazi au ajira kwa sababu hawana vyeti kamili vya kuonyesha kuwa wamehitimu. Mwanafunzi mwingine wa Chuo Kikuu cha Kisii alieleza jinsi alivyokosa nafasi ya mafunzo ya kisheria (internship) kwa sababu alama zake hazikuwa zimeingizwa kwenye mfumo wa data. 

"Nilipoteza nafasi hiyo kwa sababu hawakuweza kuthibitisha kuwa nimehitimu. Huu ni mwaka wa pili sasa, na bado sina alama kamili za baadhi ya masomo," alisema kwa masikitiko.

Ahadi za Uongozi wa Chuo

Uongozi wa Chuo Kikuu cha Kisii umekuwa ukiahidi mara kwa mara kuwa tatizo hili litatatuliwa. Hata hivyo, licha ya ahadi hizo, hali bado haijabadilika kwa kiwango kikubwa. Wanafunzi wengi wanahisi kuna ukosefu wa uwajibikaji kutoka kwa wahadhiri na ofisi za mitihani.

Mwanafunzi mwingine, ambaye tunalibana  jina lake kwa sababu ya unyanyasaji wa kijinsia aliouona, alieleza changamoto zaidi ambazo wanafunzi wanakumbana nazo. 

"Wanafunzi wa like wanapata huduma kwa haraka zaidi kuliko wanaume, hasa vipusa. Huu ni unyanyasaji wa kijinsia ambao haupaswi kuendelea."

Wanafunzi wamekuwa wakitoa wito wa kuwekwa mifumo ya kidijitali ya kufuatilia alama zao kwa urahisi, badala ya kutegemea nyaraka za karatasi ambazo zinaweza kupotea au kucheleweshwa. 

Pia, wamependekeza kuwe na mawasiliano ya wazi kati ya wahadhiri, afisi ya mitihani, na wanafunzi, ili kutoa ufafanuzi wa mara kwa mara kuhusu hali ya alama zao.

Suala la alama kukosekana limekuwa mwiba kwa wanafunzi wengi wanaohitimu katika Chuo Kikuu cha Kisii. Matatizo haya yanasababisha msongo wa mawazo, kuchelewesha mipango ya maisha, na hata kupoteza fursa muhimu za kitaaluma. Kuna haja ya uongozi wa chuo kuweka mikakati thabiti ili kuhakikisha wanafunzi wanapata haki yao bila vikwazo vya kukosekana kwa alama.

Kwa wanafunzi, hili ni somo la uvumilivu, lakini wanasema kuwa uvumilivu huu hauna kikomo. Wana matumaini kuwa uongozi wa chuo utachukua hatua za haraka kurekebisha hali hii, ili kuwawezesha kuhitimu kwa wakati na kwa heshima waliyopata kwa juhudi zao.